PEACE

KARIBU TANZANIA/ WELCOME TO TANZANIA

Thursday, September 11, 2008

WAZIRI MKUU MH.PINDA ATAKA WATANZANIA WACHUNGUZE FURSA ZA KIBIASHARA ZILIZOPO EAC

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wafanyabiashara wa Kitanzania watakaozuru nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi wachunguze fursa zilizopo kwenye nchi hizo ili wenzao waweze kufaidika pia.Amesema hayo leo mchana wakati alipofanya mazungumzo na ujumbe wa wafanyabishara Watanzania watakaofanya ziara katika nchi hizo nne kuanzia Septemba 7-16, 2008. “Katika ziara hii mjitahidi kuangalia ni maeneo gani tuna fursa kubwa ya kushindana na wenzetu ili nasi tuwezeshe wajasiriamali wetu wengi kuingia katika biashara za kimataifa,” alisema Waziri Mkuu alipokutana nao kwenye ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.Akizungumza na wawakilishi wa wafanyabiashara 50 watakaowepo kwenye msafara huo, Waziri Mkuu alisema: “Nyie ndio wenye uwezo wa kuongoza biashara, Serikali ina jukumu la kujenga mazingira mazuri yatakayowawezesha kufanya biashara zenu kwa utulivu na amani. Na hilo nawahahakikishia tunalifanya na tutaendelea kulifanya. Ainisheni vikwazo tufahamisheni Serikalini ili tuweze kuchukua hatua za kuondoa vikwazo hivyo.” Waziri Mkuu alisema kwa kubuni na kukubali kufanya ziara hiyo, wafanyabiashara watapanua uelewa wao wa biashara, watapata mbinu mpya za kibiashara na ni pia ni wakati muafaka wa kuboresha miundombinu ya kufanya biashara zao. Wafanyabiashara hao wanatoka mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Arusha na Dar es Salaam.Aliwataka waangalie fursa za uwekezaji kwenye viwanda ambako hali si nzuri ikilinganishwa na nchi za jirani. “Hapa kwetu ni kweli tuna fursa nyingi na takwimu za uwekezaji zinaonyesha kuongezeka, lakini tujiulize kweli viwanda vikubwa tunavyo vingapi na vinazalisha kiasi gani?”Alitoa mfano wa Kenya ambayo ina viwanda vikubwa 900 na kati ya hivyo 200 ni vya wawekezaji wakubwa wa nje (Multinationals) ambavyo vinamilikiwa kwa ubia na wananchi na wawekezaji wa nje pekee.Alisisitiza haja ya kutafuta fursa za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na zile zitakawezesha kuleta mapinduzi katika kilimo. “Tunahitaji kuanza kilimo cha mashamba makubwa yanayotumia teknolojia za kisasa zenye tija, yaani Kilimo cha Kibiashara (Commercial Farming).Akitolea mfano sekta hiyo, alisema Kenya wameanza kilimo hiki muda mrefu kwa vile wana mashamba makubwa ya Kahawa, Nafaka, Maua na Chai. “Pia, Kenya na Uganda wana uzoefu mkubwa wa kuzalisha mbegu bora za nafaka… Tanzania tunaagiza asilimia 75 ya mahitaji yetu ya mbegu bora kutoka nje na sehemu kubwa inaagizwa kutoka Kenya… hili ni eneo muhimu sana ambalo tunapaswa kujifunza kutoka kwao ili tubadili kilimo chetu kiwe cha tija kubwa na cha kibiashara.”Aliwasihi wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kushiriki katika ziara hii ambayo, alisema ni ziara itakayoandika historia mpya kwa wafanyabiashara wa Tanzania. “Ni ziara ya kuwafungua macho wafanyabiashara. Ni ziara ya kujifunza na kuwafanya wafanyabiashara kujiamini zaidi,” alisisitiza.Alisema mbali na kuangalia nchi hizo nne za Afrika Mashariki, wafikirie pia soko la SADC kwa sababu Tanzania ni wanachama wa jumuiya hiyo na akawakumbusha wasiisahau nchi ya DRC kwani ina wakazi zaidi ya milioni 60. “… hili nalo ni soko kubwa na eneo la kibiashara na uwekezaji, tuandaae mkakati wa kutambua fursa zilizopo katika Ukanda wa SADC bila kuwasahau jirani zetu wa DRC… Tuondokane na mawazo potofu kuwa masoko yako kwenye nchi zilizoendelea tu,” alisema. Wakiwa katika ziara hiyo, wafanyabiashara hao wanatarajiwa kujikita zaidi katika sekta saba ambazo ni miundombinu yaani barabara, reli na usafiri wa angani na majini (Infrastructure Development of Airports, Seaports and General Transportation); Nishati na Madini (Energy & Mining) na Biashara (Trade – Import/Export).Nyingine ni Usindikaji na biashara ya mazao (Agribusiness); Hoteli na Utalii (Hotel & Tourism); Viwanda, Ujenzi na Uhandisi (Manufacturing, Construction & Engineering); na Sekta ya Huduma za Fedha (Financial Services).

1 comment:

Anonymous said...

Bongo porojo haziishi tu!!