WASOMI wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kusimamia kwa ukali na umakini mkubwa ili kuhakikisha watu walioshiriki katika ufisadi uliokithiri katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wanarudisha fedha zote zilizoibwa na wahusika kuchukuliwa hatua.
Hayo yalisemwa jana na Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Deo Daudi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kuwa utekelezaji wa suala hilo utaliletea heshima taifa katika mapambano dhidi ya rushwa.
Rais huyo wa Daruso alisema kuwa, aliyekuwa Gavana wa BoT, Dk. Daudi Balali na wenzake kutokomeza zaidi ya sh bilioni 133 ni dhambi.
Alisema kuwa wizi wa kiasi hicho cha fedha ni sawa na kubomoa vituo vyote vya afya Tanzania, au kuiba fedha za kuwasomesha wanafunzi wote wa elimu ya juu ndani na nje ya nchi kwa miaka kadhaa.
“Tunampongeza Rais Kikwete tukiamini sasa ameamua kushughulikia suala hili la rushwa bila kusimama, kwa maana hii ndiyo njia pekee ya kuwanasua Watanzania kutoka katika lindi la umaskini ambao wengi tunaona ni wa kuaminishwa zaidi ili kuwapisha akina Balali kutuibia,” alisema Daudi.
Alisema ufisadi haupo BoT pekee na kumtaka Rais Kikwete kugeukia kwenye taasisi nyingine pia.
“Tunamtaka rais aongeze kasi ya kupambana na watu hawa ambao wana dhambi kubwa isiyosameheka ya kuwafanya Watanzania kuwa maskini wa kutupwa katikati ya utajiri uliopindukia,” alisema rais huyo wa Daruso.
Pia alimkumbusha Rais Kikwete na kumtaka kuutambua mchango wa vyombo vya habari katika vita dhidi ya ufisadi na rushwa.
Tuesday, July 22, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment