PEACE

KARIBU TANZANIA/ WELCOME TO TANZANIA

Wednesday, August 13, 2008

Mramba amlipua Mkapa!

Katiaka kile ambacho pengine hakikutazamiwa kutokea, Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa na ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rombo, Mheshimiwa Basil Mramba, amemlipua kiaina Rais Mstaafu Mkapa kwa kuiponda Serikali yake kuhusu sera ya viwanda. Mheshimiwa Mramba amesema Serikali hiyo ya awamu ya tatu ( iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mkapa), kamwe haikuwahi kutekeleza sera ya viwanda. Akizungumza bungeni jana wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Mheshimiwa Mramba akazidi kueleza kuwa kwa kasi iliyokuwepo katika serikali ya awamu ya tatu, nchi ingechukua muda mrefu sana kuwa na viwanda. ``...Nina tatizo. Najua watu watauliza, si (nawe) ulikuwepo. Lakini wacha niseme,`` ndivyo alivyoanza kueleza Mheshimiwa Mramba kabla ya kuchangia zaidi. Aidha, Mheshimiwa Mramba aliwageukia wajumbe wa Halmashauri ya CCM ,NEC na kuwahoji kuhusu sera ya viwanda vidogovidogo. ``Simuoni Bw. Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wetu wa CCM... lakini nawaona wajumbe wengi wa Halmashaurii Kuu ya Taifa. Nauliza, hivi CCM ina Sera ya viwanda vidogo vidogo?`` Akahoji Mheshimiwa Mramba ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Akasema viwanda vilivyopo sasa ni matokeo ya sera za Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Rais wa wakati huo, Marehemu Mwalimu Nyerere. Akasisitiza kuwa viwanda vingi vilivyopo leo ni vya Nyerere na kwamba sera yake ilikuwa ni viwanda vya awali, ambayo amesema kamwe haijatekelezwa katika serikali ya awamu ya tatu (ya Rais Mkapa). Hata hivyo, Mheshimiwa Mramba akasema anafurahia kuona Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko ameipeleka bungeni, huku akishauri kuwa Serikali ya sasa ya awamu ya nne, ijielekeze katika jitihada za kuchochea uanzishaji wa viwanda. Pia akaishauri serikali kusamehe kodi kwa viwanda vidogo vidogo kama inavyofanya kwa viwanda vikubwa ambavyo vimekuwa vikipata msamaha. Aidha, ametaka kuanzishwa kwa benki maalum kwa ajili ya viwanda vidogo ama kuziagiza benki kutenga fungu maalum kwa ajili ya kuwakopesha wanaoanzisha viwanda hivyo.

SOURCE: Alasiri

No comments: